Mashambulizi ya marekani
Marekani imesema kuwa imetekeleza mashambulizi zaidi kazkazini mwa Iraq dhidi ya maeneo yanayodhibitiwa na wapiganaji wa Jihad.
Taarifa kutoka Pentagon imesema kuwa ndege za
Marekani pamoja na zile zisizo na rubani ziliharibu magari ya kijeshi ya
wanamgambo hao likiwemo lile lilokuwa likiwashambulia raia wa Yazidi
ambao wamekimbilia hifadhi katika mlima Sinjar.
Awali Rais Obama amesema kuwa
kupitia washirika wake wa ulaya pamoja na wanajeshi wa Iraq watawakabili
wanamgambo ambao wameuzunguka mlima huo.
Hatahivyo ameonya kuwa kampeni hiyo ya kijeshi
itachukua miezi kadhaa na kwamba itachukua mda kwa jeshi la Iraq
kujikusanya ili kutoa upinzani mkali dhidi ya wanamgambo hao.
Ndege za marekani zilizobeba misaada nchini Iraq
Wakati huohuo Ndege za kijeshi za Marekani na
zile za Uingereza zimeendelea kuangusha misaada kwa raia waliokwama
katika Mlima Sinjar nchini Iraq,ijapokuwa viongozi wa mataifa hayo
mawili wamekubaliana kwamba hatua hiyo sio suluhu ya kudumu.
Wamesema kuwa lazima njia ya kuwaondoa raia hao hadi katika eneo lililo salama itafutwe ili kuzuia mauaji ya kimbari.
Mfanyikazi mmoja wa shirika la Amnesty
International kazkazini mwa Iraq, Donatella Rovera ameiambia BBC kwamba
maelfu ya raia kazkazini na magharibi mwa mlima huo wamefanikiwa
kutoroka,lakini wengi zaidi katika eneo la kusini la mlima huo hawana
mahala pa kwenda.
Amesema kuwa wale waliotoroka wako katika hali mbaya baada ya kukaa siku sita bila chakula na maji kidogo.